Follow by Email

Friday, August 31, 2012

Rais Kikwete atuma Salamu za Rambirambi kwa Familia ya Mama Hawa Ngulume


THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS

Telephone: 255-22-2114512, 2116898
              press@ikulu.go.tz             

Fax: 255-22-2113425


PRESIDENT’S OFFICE,
      THE STATE HOUSE,
              P.O. BOX 9120,  
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
 


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ametuma Salamu za Rambirambi kwa Familia ya aliyepata kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Mama Hawa Ngulume kufuatia taarifa za kifo chake kilichotokea katika Hospitali ya Jeshi Lugalo, Jijini Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kwa matibabu akisumbuliwa na ugonjwa wa Saratani.  Mama Hawa Ngulume amefariki leo tarehe 30 Agosti, 2012.

Katika Salamu zake hizo, Rais Kikwete amesema Marehemu Hawa Ngulume, enzi za uhai wake, alikuwa kiongozi shupavu aliyesimamia maamuzi yake katika majukumu muhimu ya kitaifa kwa lengo la kuwaletea  wananchi maendeleo katika sehemu zote alizotumikia akiwa Mtumishi wa Umma, na baadaye alipopewa wadhifa wa Mkuu wa Wilaya alioutumikia katika Wilaya za Singida Mjini katika Mkoa wa Singida, Kinondoni Mkoani Dar es Salaam na mara ya mwisho katika Wilaya ya Mbarali, Mkoani Mbeya.

“Nilimfahamu Marehemu, enzi za uhai wake, kama Kiongozi Mwanamke shupavu aliyesimamia kikamilifu maamuzi yake, na hivyo kuthibitisha ukweli kwamba wanawake wakipewa fursa wanaweza”, amesema Rais Kikwete katika kuomboleza kifo chake.

“Kutokana na msiba huo mkubwa, natuma Salamu za Rambirambi kutoka dhati ya moyo wangu kwa Familia ya Marehemu, Mama Hawa Ngulume kwa kuondokewa na Mhimili muhimu na Kiongozi wa Familia.  Natambua machungu mliyo nayo hivi sasa kwa kumpoteza Mama wa Familia, lakini nawahakikishia kuwa niko pamoja nanyi katika kuomboleza msiba huu mkubwa”, ameongeza kusema Rais Kikwete katika Salamu zake.

Rais Kikwete amewataka wanafamilia ya Marehemu wawe na moyo wa uvumilivu na ujasiri wakati huu wanapoomboleza msiba wa mpendwa wao kwani yote ni Mapenzi yake Mola.  Amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aipokee na kuilaza mahala pema peponi Roho ya Marehemu Mama Hawa Ngulume, Amina. 

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
30 Agosti, 2012

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.