Follow by Email

Monday, August 27, 2012

Mkutano wa NAM waanza nchini Iran


 
Na Ally Kondo,
Tehran, Iran

Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikari wa Nchi Zisizofungama na Upande Wowote (NAM) umeanza jijini Tehran, Jamhuri ya Kiislam ya Iran siku ya Jumapili, tarehe 26 Agosti 2012. Mkutano huo utakaoisha tarehe 31 Agosti 2012 umeanza na kikao cha wa Wataalam ambacho kitafuatiwa na Mkutano wa Mawaziri tarehe 28 na 29 Agosti 2012 na kisha ule wa Wakuu wa Nchi na Serikali tarehe 30 na 31 Agosti 2012.

Katika Mkutano wa Wataalam, Ujumbe wa Tanzania unajumuisha Balozi Celestine Mushy, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dkt Justin Seruhere, Kaimu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa, New York, pamoja na maafisa wengine kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

Mheshimiwa Dkt. Mohammed Gharib Bilal, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atamwakilisha Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali.

Wakati wa ufunguzi wa kikao cha wataalam, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Dkt. Ali Akbar Salehi alieleza kuwa nchi yake ambayo imechukuwa Uenyekiti wa NAM kutoka kwa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri katika kipindi cha miaka mitatu ijayo, itajitahidi kuhakikisha kuwa Umoja huo unaendelea kuimarika katika kutekeleza malengo yake ya msingi. Waziri huyo aliendelea kueleza kuwa kufanyika kwa Mkutano huo ni ishara ya wazi kuwa NAM ina dhamira ya dhati ya kuuenzi umoja huo na kuufanya kuwa chombo madhubuti cha  kutetea na kulinda maslahi ya wanachama wake.

Mhe. Salehi alifafanua baadhi ya masuala ambayo NAM imekuwa ikiyapa umuhimu mkubwa tangu kuundwa kwake mwaka 1961 na yanayotakiwa kundelea kupewa kipaumbele ni pamoja na: kutambua na kuheshimu tofauti za tamaduni duniani na kupinga jitihada zozote za kupandikiza tamaduni za kigeni zisizokubalika katika nchi nyingine.

Hivyo, alibainisha kuwa NAM inafanya juhudi kubwa kufanya majadiliano miongoni mwa jamii, tamaduni na dini tofauti kwa lengo la kukuza na kuimarisha ushirikiano, amani na kuondoa ubaguzi.

Waziri huyo alibainisha kwamba nchi zote duniani zinauona Umoja wa Mataifa kuwa ni Taasisi kubwa ulimwenguni ambayo iliundwa kutokana na athari za Vita Kuu vya pili vya dunia. Hivyo, wanachama wa NAM hawaungi mkono masuala yote ambayo yanatokea duniani yenye dhamira ya ukandamizaji kama vile dhuluma, ubaguzi, matumizi mabaya ya madaraka, ubabe, aina zote za ukoloni pamoja na mizozo inayohusisha matumizi ya silaha.

Aidha, Mhe. Salehi katika hotuba yake aligusia masuala ambayo yanajiri hivi sasa duniani, hususan Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika. Alisisitiza umuhimu wa kusikiliza ujumbe unaotolewa na watu wa maeneo hayo ambao wanapigania uhuru, haki na utu. Alisema kuwa mafunzo yanayopatikana kutokana na vitendo hivyo ni kwamba hakuna utawala ambao unaweza kupuuza matakwa na malengo halali ya watu wake. Hivyo, njia pekee ya kuepukana na masuala hayo ni tawala za kiimla zikubali kufanya majadiliano, kuheshimu haki za msingi za binadamu na kutimiza mahitaji ya msingi ya watu wao.

Kuhusu mradi wa nyuklia wa Iran, Waziri Salehi alisema kuwa mpango huo ni wa amani na hauna lengo la kutengeneza silaha za nyuklia. Alisisitiza kuwa Iran ipo tayari wakati wowote kushirikiana na upande wowote katika masuala yanayohusu masuala ya nyuklia na ambayo hayakiuki haki na wajibu wa nchi. Alisisitiza msimamo wa nchi yake kwamba haitafuti mzozo wowote au kitu chochote kile zaidi ya haki zake za kimsingi ambazo haziwezi kuzuiliwa na mtu yoyote.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.