Follow by Email

Wednesday, June 13, 2012

Rais Kikwete apokea hati za utambulishoRais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatano, Juni 13, 2012, amepokea hati za utambulisho kutoka kwa mabalozi watano watakaoziwakilisha nchi zao katika Tanzania. Mabalozi wote watano wana makazi yao mjini Nairobi, Kenya.

Mabalozi waliowasilisha hati zao za utambulisho katika halfa zilizofanyika Ikulu, Dar es Salaam ni Balozi wa Philippines Mheshimiwa Domingo D. Lucenario, Balozi wa Ukraine Mheshimiwa Volodymyr Butiaha, Balozi wa Eritrea Mheshimiwa Beyene Russom Habtai, Balozi wa Ghana Mheshimiwa Kingsley Saka A. Karimu na Balozi wa Israel Mheshimiwa Gil Haskel.

Akizungumza na Balozi wa Philippines baada ya kuwa amepokea hati zake za utambulisho, Rais Kikwete amekubaliana na ombi la nchi hiyo kuteua balozi wa heshima ambaye atakuwa anafuatilia maslahi ya siku kwa siku ya nchi hiyo mjini Dar es Salaam ,kwa sababu Balozi Lucenario ana makazi yake mjini Nairobi, Kenya.

Rais Kikwete pia amemtaka Balozi Lucenario kusaidia kuyashawishi makampuni ya Philippines kuja kuwekeza nchini hasa katika maeneo ambako nchi hiyo ina ujuzi mkubwa kama vile uvuvi.

“Tuna eneo kubwa la bahari ambalo halitumiki kabisa kwa ajili ya uvuvi ambako samaki watavuliwa kisayansi na kwa namna ya kupata samaki wa kukidhi mahitaji ya ndani ya nchi na kutuwezesha kuuza nje,” Rais Kikwete amemwambia Balozi Lucenario.

Naye Balozi Butiaha wa Ukraine amemwambia Rais Kikwete kuwa nchi yake inapenda kuwahimiza wafanyabiashara wa nchi hiyo kuja kuwekeza katika uchumi wa Tanzania hasa katika maeneo ya usafirishaji, ulinzi, uendeshaji wa rasilimali za maji, mawasiliano, utengenezaji wa mabasi ya abiria, utengenezaji wa mabehewa ya treni, kuwekeza katika usafishaji maji kama wafanyabiashara hao walivyofanya katika nchi nyingine.

Balozi huyo amemwambia Rais Kikwete: “ Katika Nigeria tumewekeana mkataba wa kujenga kiwanda cha kufua chuma, katika Iran tumewekeza katika kiwanda cha kutengeneza ndege na katika Gambia tumewekeza katika utengenezaji wa meli na vyombo vingine vya bahari. Tunataka kufanya hivyo hapa kwa kushirikiana na wawekezaji wa ndani ili kuibua fursa za ajira.”

Katika mazungumzo na mabalozi wa Eritrea na Ghana, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania imedhamiria kuendeleza uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na nchi hizo mbili.

“Uhusiano wa Tanzania na Ghana ulianza miaka mingi toka enzi za Mwalimu Julius Nyerere na Kwame Nkurumah, wajibu wetu ni kuuendeleza, kuukuza na kuuboresha,” Rais Kikwete amemwambia Balozi Karimu wa Ghana.

Katika mazungumzo na Balozi Haskel wa Israel, Rais Kikwete ametaka Israel kuisaidia Tanzania kukuza kilimo cha matunda na mboga, eneo ambako nchi hiyo ya Mashariki ya Kati ina ujuzi na utaalam mkubwa.

Rais Kikwete pia ametumia muda mfupi kumweleza hali iliyoko Zanzibar kufuatia ghasia na fujo za karibu zilizofanywa na kikundi cha Uamsho katika Kisiwa hicho.

“Kama kweli kikundi cha Uamsho hakitaki Muungano basi siyo hoja; kiende kwenye Tume ya Katiba ambayo tayari tumeiunda ili kieleze msimamo wake. Hakuna ugomvi na hili. Isingekuwepo Tume tungeweza kuelewa, lakini tumekwisha kuunda Tume, wakatoe maoni yao huko. Lakini kufanya fujo na kuendesha vitendo vya mapambano hakuna faida. Wanachohubiri siyo tena dini bali ni ajenda ya kisiasa,” Rais Kikwete amemwambia  Balozi Haskel.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.