Follow by Email

Thursday, April 26, 2012

MKUTANO WA BARAZA LA MAWAZIRI WA EAC


Mhe. Bernard K. Membe (Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (wa katikati mstari wa mbele) akiwa na Mhe. Hussein Mwinyi (Mb.), Waziri wa Ulinzi pamoja na Mhe. Harrison Mwakyembe (Mb.), Naibu Waziri wa Ujenzi kwenye moja ya vikao vya majadiliano vya ujumbe wa Tanzania kabla ya Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika mjini Arusha tarehe 25 Aprili, 2012. (Picha na Wizara ya Mambo ya Nje).


Mabalozi wa Tanzania katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa katika moja ya vikao vya majadiliano wakati wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo uliofanyika jana mjini Arusha. Kutoka kushoto ni Dkt. Batilda Buriani, Balozi wa Tanzania, Kenya, Mhe. Marwa Matiko, Balozi wa Tanzania, Rwanda, Mhe. James Nzagi, Balozi wa Tanzania, burundi na Mhe. Dkt. Ladislaus Komba, Balozi wa Tanzania, Uganda.


Mhe. Samwel Sitta, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara yake, Dkt. Stergomena Tax-Bamwenda akiongoza moja ya vikao vya majadiliano vya ujumbe wa Tanzania (haupo pichani) kabla ya Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo uliofanyika Arusha tarehe 25 Aprili, 2012.


Bw. John Haule, Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akibadilishana mawazo na Bw. George Masaju, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wa Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki jana mjini Arusha.


Mhe. Samwel Sitta, Waziri wa Afrika Mashariki, akiwa na baadhi ya Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakisaini Ripoti  baada ya kufikia makubaliano katika mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya hiyo uliofanyika jana mjini Arusha. 

26 Aprili, 2012
Na ROSEMARY MALALE, ARUSHA
Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umefanyika mjini Arusha jana kujadili na kukubaliana agenda mbalimbali zitakazowasilishwa kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo tarehe 28 Aprili, 2012.

Miongoni mwa agenda muhimu zilizojadiliwa na Mawaziri hao ni pamoja na mapendekezo ya kuteua Naibu Katibu Mkuu  mpya kutoka Uganda kufuatia aliyekuwepo Bibi Beartice Kiraso kumaliza muda wake; kuongeza mkataba wa miaka mitatu kwa Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Bw. Jean Claude Nsengiyumva kutoka Burundi; kupitia ripoti kuhusu maombi ya Jamhuri ya Sudan Kusini ya kuwa mwanachama wa Jumuiya na kupitia Mswada wa sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuhusu uangalizi wa uzito wa mizigo inayobebwa na magari ili kulinda barabara za nchi wanachama zisiharibiwe.
Masuala mengine yaliyojadiliwa ni Rasimu ya Itifaki ya Kupambana na Rushwa kwa nchi wanachama; Rasimu ya Itifaki ya Ushirikiano katika masuala ya Ulinzi na ripoti ya Kamati ya Fedha na Utawala.
Awali akifungua Mkutano huo wa Baraza la Mawaziri, Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Dkt. Richard Sezibera aliwaomba Mawaziri watoe maoni yao kuhusu agenda hizo ili baadae zifikishwe na kuridhiwa na Wakuu wa Nchi.
Mkutano huo wa Mawaziri ulitanguliwa na vikao vya Maafisa Waandamizi kutoka nchi wanachama kilichofanyika tarehe 20-22 Aprili kikifuatiwa na kikao cha Kamati ya Uratibu chini ya Makatibu Wakuu kutoka nchi wanachama kilichofanyika tarehe 23 na 24 Aprili, 2012.
Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo  uliongozwa na Mhe. Samwel Sitta (Mb), Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kuwahusisha pia Mhe. Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Hussein Mwinyi (Mb), Waziri wa Ulinzi, Mhe. Perreira Ame Silima (Mb), Naibu Waziri wa Fedha na Mhe. Harrison Mwakyembe (Mb), Naibu Waziri wa Ujenzi.
Wengine ni Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. George Masaju, Dkt. Stergomena Tax-Bamwenda, Katibu Mkuu wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. John Haule, Katibu Mkuu wa Mambo ya  Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Herbert Mrango, Katibu Mkuu wa Ujenzi, Bw. Job Masima, Katibu Mkuu wa Ulinzi, Mabalozi wa Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi na Maafisa Waandamizi  kutoka Serikalini.
Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utafanyika mjini hapa tarehe 28 Aprili, 2012.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.