Follow by Email

Sunday, April 29, 2012

Wakuu wa Nchi wa EAC wasaini Itifaki ya Mkataba wa masuala ya UlinziMhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete (wa pili kushoto), akiwa na viongozi wenzake wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakitia saini Mkataba wa makubaliano ya ushirikiano katika ulinzi.  Sherehe hiyo ilifanyika Ngurdoto Lodge tarehe 28 Aprili, 2012.  (picha na Ikulu)

Na ROSEMARY MALALE, Arusha
28 Aprili, 2012
Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wameridhia na kusaini Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Ushirikiano katika masuala ya Ulinzi na kuelekeza kuanza mara moja kwa  majadiliano ya pamoja yatakayopelekea kukamilika kwa Mkataba wa Pamoja katika masuala ya Ulinzi.
Aidha, mbali na kutia saini Itifaki hiyo Wakuu hao wa Nchi waliipokea ripoti iliyowasilishwa kwao na Baraza la Mawaziri na kuridhia masuala mbalimbali katika ripoti hiyo ikiwa ni pamoja na kumteua Bi. Jesca Eriyo, kutoka Uganda kuwa Naibu Katibu Mkuu mpya  kufuatia aliyekuwepo Bibi Beartice Kiraso kumaliza muda wake wa kazi katika Jumuiya.
Vilevile Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo waliridhia pendekezo la kumuongezea mkataba wa miaka  mingine mitatu  Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo Bw. Jean Clausde Nsengiyumva kutoka Burundi.
Kuhusu maombi ya Sudan Kusini ya kuwa Mwanachama wa Jumuiya hiyo, wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekubali mapendekezo ya Baraza la Mawaziri ya kuundwa kwa Timu ya Uhakiki itakayohusisha wataalam watatu kutoka kila nchi mwanachama na Wataalam watatu kutoka katika Sekretarieti ya Jumuiya hiyo kwa ajili ya kuwezesha zoezi hilo.
Timu hiyo ya uhakiki, pamoja na mambo mengine itapitia maombi ya nchi hiyo na kuona kama yanakidhi Vigezo vya Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuwa mwanachama. Vigezo hivyo ni pamoja na masuala ya kijiografia yaani kama nchi ya Sudan Kusini inapakana au ipo karibu na mojawapo ya nchi mwanachama wa jumuiya hiyo;   nchi kuzingatia kanuni na misingi ya kimataifa ya demokrasia, utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu, utawala bora na mchango wan chi katika kuimarisha ushirikiano ndani ya Jumuiya.
Wakuu hao wan chi pia walizungumzia masuala ya usalama katika kanda ya Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na mgogoro unaoendelea baina ya Sudan na Sudan Kusini na kuzitaka nchi hizo kurudi kwenye meza ya mazungumzo kumaliza tofauti zao.
Awali akifungua mkutano huo, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Tanzania na mwenyeji wa mkutano aliwakaribisha nchini marais na viongozi mbalimbali kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kueleza kuwa ni imani yake kuwa mkutano huo utakuwa ni wa mafanikio makubwa kwa manufaa ya wananchi wa Afrika Mashariki kwa ujumla.
“Sitapenda kuchukua muda mwingi kuzungumza siku ya leo bali nawakaribisha sana Tanzania na hasa hapa Arusha na ni imani yangu kuwa mkutano huu utakuwa wa mafanikio na manufaa kwa wananchi wa Jumuiya hii,” alisema Mhe. Kikwete.
Aidha, katika hotuba yake Mhe. Mwai Kibaki, Rais wa Kenya  ambaye pia ni Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya hiyo alieleza kuwa kuna umuhimu kwa nchi wanachama kuimarisha na kuwa na mtandao wa pamoja  wa miundombinu ili kukuza biashara na uchumi kwa ujumla.
Mkutano huo Maalum wa 10 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ulifanyika mjini Arusha tarehe 28 Aprili, 2012 na kuhudhuriwa na Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Tanzania, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Uganda, Mhe. Mwai Kibaki, Rais wa Kenya na Mhe. Paul Kagame, Rais wa Rwanda.
Wengine ni Mhe. Therence Sinunguruza Makamu wa Kwanza wa Rais wa Burundi, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa hapa nchini na wadau mbalimbali.

-Mwisho-

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.