Follow by Email

Monday, February 13, 2012

Mhe Rais akutana na Mwakilishi Maalum wa Rais wa Urusi


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amekutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Mikhail V. Margelov, Mjumbe Maalum wa Rais wa Urusi, Mheshimiwa Dmitry Medvedev.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo, Jumatatu, Februari 13, 2012 Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete amemtaka Mjumbe Maalum huyo kusaidia kushawishi makampuni zaidi ya Urusi kuwekeza katika uchumi wa Tanzania.
Aidha, Rais Kikwete ametaka Tanzania na Urusi kuongeza ushirikiano wa kiuchumi katika nyanja mbali mbali ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua ambazo zitaongeza idadi ya watalii wa Urusi wanaotembelea Tanzania. Mwaka jana ni watalii 4,500 wa Urusi waliotembelea Tanzania.
Rais Kikwete na Mheshimiwa Margelov pia wamezungumzia masuala mbali mbali ya kimataifa, ya kanda ya Afrika na ya uhusiano kati ya Tanzania na Urusi.
Mjumbe Maalum huyo wa Mheshimiwa Medvedev anatembelea Tanzania ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika nchi za Afrika Mashariki za Kenya na Uganda. Alianza ziara yake kwa kutembelea Zanzibar jana na atakuwa Kenya kesho.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.