Follow by Email

Thursday, September 8, 2011

Mhe. Membe akutana na Mabalozi nchini


Mheshimiwa Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa leo Jumatano Septemba 7, 2011 amekutana na Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa hapa nchini kwenye ukumbi wa Karimjee.

Katika mkutano huo, Waziri Membe amezungumzia tatizo la umeme nchini na kufafanua mikakati ya Serikali katika kukabiliana na tatizo hilo. Alisema Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imeweka mkakati wa muda mfupi ambapo kwa kutumia umeme wa gesi, kutakuwa na ongezeko la megawati mia sita kati ya Disemba 2011 hadi Disemba 2012.

Kupitia mkutano huo, Mhe. Waziri Membe alieleza kwamba suala muhimu katika mgogoro wa Libya si Umoja wa Afrika au Tanzania kulitambua Baraza la Mpito la Libya (NTC) kama nchi za Magharibi zinavyotaka bali Baraza hilo kutambua na kutekeleza roadmap for peace iliyowekwa na Umoja wa Afrika mjini Malabo, Equitorial Guinea kuhakikisha amani ya kudumu inapatikana nchini humo.

“Tanzania inawapenda sana watu wa Libya na taifa lao, tunataka kuona taifa hilo likishamiri na kurudi kwenye hali ya utulivu na amani ili wananchi wa Libya waendelee kujenga taifa lao” alisema Waziri Membe.

Kuhusu baa la njaa lililoikumba Somalia, Mhe. Waziri Membe aliwaambia mabalozi hao kuwa Serikali ya
Tanzania imetoa msaada wa chakula na misaada mingine ya kibinaadam kwenda nchini humo. Aliishukuru Serikali ya Afrika Kusini kwa kusaidia kusafirisha misaada hiyo kwa ndege hadi Mogadishu, Somalia.

Mwisho, Waziri Membe aliwaarifu mabalozi hao kuhusu nia ya Wizara yake ya kusherehekea miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika kwa kuwapeleka Mabalozi safari ya kuitambua Tanzania na vivutio vyake. Safari hiyo inayotarajiwa kufanywa mwanzoni mwa mwezi Oktoba, itaanzia Butiama, nyumbani kwa Baba wa Taifa, Hayati Julius Kambarage Nyerere na kuishia Zanzibar, nyumbani kwa aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Zanzibar Hayati Abeid Amani Karume.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
Septemba 7, 2011

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.