Follow by Email

Saturday, April 25, 2015

Waziri Membe apokea Nakala za Hati za Utambulisho kutoka Mabalozi Wateule wa Urusi na Algeria

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb), akipokea Nakala za Hati za Utambulisho za Balozi Mteule wa Urusi nchini Tanzania, Mhe. Yuri Fedorovich Popov.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb). akiwa katika mazungumzo na Balozi Mteule wa Urusi mara baada ya kupokea Nakala za Hati za Utambulisho. Katika mazungumzo hayo pamoja na mambo mengine, Mhe. Waziri aliishukuru Serikali ya Urusi kwa misaada inayotoa kwa Tanzania katika sekta mbalimbali kama vile elimu. Wawili hao pia waliafikiana  umuhimu wa kukuza na kuimarisha zaidi ushirikiano kati ya Tanzania na Urusi.
Mazungumzo yanaendelea.
Waziri Membe akiagana na Balozi Mteule wa Urusi nchini Tanzania.
Waziri Membe katikati akiwa katika picha ya pamoja na Balozi Mteule wa Urusi. Wakwanza kulia ni Balozi Joseph Sokoine, Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na kutoka kushoto ni maafisa wa Ubalozi wa Urusi nchini Tanzania.

============================================

BALOZI MTEULE WA ALGERIA
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb), akipokea Nakala za Hati za Utambulisho za Balozi Mteule wa Algeria nchini Tanzania, Mhe.Saad Belabed.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb) akiwa katika mazungumzo na Balozi Mteule wa Algeria nchini Tanzania. Katika mazungumzo hayo, Mhe. Membe alieleza kuwa zaidi ya miaka 50 sasa Tanzania na Algeria zimekuwa katika uhusiano na ushirikiano mzuri wa nchi na nchi na hata katika ngazi ya Kimataifa kama vile Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.
Mazungumzo yakiendelea
Mazungumzo yanaendelea huku Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa (wa kwanza kushoto), Bi. Zuhura Bundala na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Bi. Mindi Kasiga wakinukuu mazungumzo hayo.
Waziri Membe akiagana na Balozi Mteule wa Algeria nchini Tanzania baada ya kupokea Nakala za Hati za Utambulisho.

Picha na Reginald Philip.


Friday, April 24, 2015

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje akutana kwa mazungumzo na CEO wa Standard Chartered nchini

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Dkt. Mahadhi Juma Maalim (Mb.) akimkaribisha Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered nchini Bi. Liz Lloyd alipomtembelea Wizarani kwa ajili ya mazungumzo na Mhe. Maalim. 
Mhe. Maalim akimtambulisha kwa Bi. Llyoid Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Simba Yahya. 
Mhe. Dkt.  Maalim akizungumza na Bi. Lloyd
Ujumbe alioambatana nao Bi. Lloyd wakifuatilia mazungumzo.
Bi. Lloyd nae alipata wasaa wa kuchangia hoja wakati wa mazungumzo na Dkt.  Maalim 
Balozi  Yahya (kushoto) akiwa na Katibu wa Naibu Waziri Bw. Adam Isara wakisikiliza mazungumzo kati ya Dkt. Maalim na Bi. Lloyd (hawapo pichani)
Mazungumzo yakiendelea.


Picha na Reginald Kisaka.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje amuaga Mwakilishi wa FAO nchini

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Mahadhi Juma Maalim (Mb.) akimkaribisha Mwakilishi wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (F.A.O) nchini Bi. Diana E. Tempelman alipomtembelea ofisini kwake kwa ajili ya kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa uwakilishi wa Shirika hilo hapa nchini. 
Mhe. Dkt. Mahadhi akizungumza na Bi. Diana kwa kumpongeza kwa uwakilishi wake mzuri wa Shirika la FAO hapa nchini
Bi. Diana nae akitoa neno la shukrani kwa Naibu Waziri kwa Ushirikiano mzuri aliokuwa akiupata kutoka Wizarani wakati wote akiwa hapa nchini.  

Picha na Reginald Philip

Wednesday, April 22, 2015

Waziri Membe azungumza na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa UN eneo la Maziwa Makuu

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Bernard K. Membe (Mb.), akizungumza na Mwakilishi  Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu, Bw.  Said Djinnit walipokutana kwa mazungumzo tarehe 22 Aprili, 2015. Katika mazungumzo yao waligusia masuala ya usalama katika Ukanda huo hususan hali ilivyo nchini DRC.
Waziri Membe akimweleza jambo Bw. Said Djinnit (katikati) huku Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa na Mwakilshi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Bw. Alvaro Rodriguez akisikiliza kwa makini.
Waziri Membe (kulia) akiagana na Bw. Said Djinnit mara baada ya kumaliza mazungumzo yao


Picha na Reginald Philip

Tuesday, April 21, 2015

Watanzania 18 warejeshwa nchini kutokea Yemen

Kiongozi wa Msafara wa Watanzania waliorejeshwa nchini kutokea Yemen Bw. Abdul Twahid Said akizungumza na Waandishi wa Habari  kwa niaba ya wenzake mara baada ya kuwasili leo kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere  jijini Dar es Salaam kwa ndege ya Shirika la Emirates. Bw. Said alitoa shukrani kwa jitihada za Serikali za kuwarejesha nchini Watanzania wote kufuatia machafuko yanayoendelea nchini Yemen.
 Bw. Sabri Hery Omari ambaye ni miongoni mwa Watanzania waliorejea nae  akizungumza na Waandishi wa Habari huku sehemu nyingine ya Watanzania hao wakionekana kwa nyuma.
Watanzania waliurudishwa Nchini wakitokea nchini Yemeni kutokana na machafuko yanayoendelea huko wakifurahi kuwa nyumbani salama
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bi. Mindi Kasiga akizungumza mara baada ya Watanzania hao kuwasili nchini. Anayeonekana pembeni mwenye miwani ni Bw. Elibariki Maleko, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye alikuwepo wakati wa mapokezi hayo


Picha na Reginald Philip
============================================


Na. Reuben Mchome

Watanzania kumi na nane warejea kutoka Yemen.

Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikiwa kuwarejesha nyumbani jumla ya Watanzania kumi na nane kutoka nchini Yemen kufuatia mapigano yanayoendelea nchini humo ya wenyewe kwa wenyewe.

Watanzania hao ambao wamewasili nchini leo kwa ndege ya shirika la emirates namba EK 725 wameishukuru serikali kutokana na jitihada za haraka zilizofanywa kupitia ubalozi wa Tanzania nchini Oman na kufanikiwa kuwarejesha salama pasipo gharama zozote .

Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya Watanzania hao Bw. Sabri Abeid Almaghi ambaye alikua anafanya biashara nchini Yemen amesema kuwa anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa namna ya pekee kwa kuwajali wananchi wake bila kujali wapo nchini au nje ya nchi na kutoa msaada  kwa wakati.

“Tunaishukuru sana serikali yetu ya Tanzania kwa jinsi ambavyo wanajali wananchi wake bila kujali wapo ndani au nje ya nchi,  kweli kama sio jitihada za ubalozi wetu pale mjini Muscat, sijui leo tungekua katika hali gani, tunaomba shukrani zetu mzifikishe kwa Rais Kikwete, Waziri Membe na wahusika wengine wote waliofanikisha kuturejesha nyumbani” alisema Mzee Saleh Mbaraka Jabri mmoja wa watanzania hao waliorejea kutoka Yemen.

Aidha, akizungumzia hali ya usalama ilivyo nchini Yemen, Bw. Almaghi amesema kuwa hali ni mbaya sana kufuatia mapigano ya anga yanayoendelea hivi sasa na muda wowote yataanza mapigano ya ardhini. Aidha amesema kuwa kufuatia hali hiyo huduma zote za kijamii pamoja na biashara zimesimama.

Akizungumza mara baada ya kuwapokea watanzania hao Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano serikalini Bi. Mindi Kasiga amesema mpaka hivi sasa watanzania ambao wamesharejeshwa nchini kutoka Yemen ni 23, kati ya   Watanzania 69 ambao wamejiandikisha  na jitihada  zinaendelea.

“Awamu ya kwanza ya Watanzania waliorejeshwa na serikali kutoka nchini Yemen ni familia moja ya watu watano ambao walirudi wiki chache zilizopita” alimalizia Bi. Mindi Kasiga.

Hivi karibuni Serikali kupitia Waziri wa Mambo  na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard Membe ilitangaza kuwarejesha nchini Watanzania waliopo Yemen kufuatia machafuko yanayoendelea nchini humo.


Tanzania yashiriki mkutano wa ushirikiano wa Afrika na Asia unaofanyika Indonesia

Mhe. Dkt. Mary M. Nagu (Mb) Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- Uratibu na Mahusiano akichangia hoja katika moja ya mijadala kwenye Mkutano wa Kuadhimisha miaka 60 ya Ushirikiano kati ya Bara la Asia na Afrika unaoendelea jijini Jakarta nchini Indonesia kuanzia tarehe 19 hadi 24 Aprili 2015. Kulia kwa Waziri ni Mhe. Aziz Mlima, Balozi wa Tanzania nchini Indonesia mwenye makazi yake ya kudumu nchini Malaysia, Bw. Khatibu Makenga, Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa pamoja na Bw. Dismas Assenga, Afisa katika Ubalozi wa Tanzania nchini Malaysia.
Mkutano huo kwa ngazi ya Mawaziri ukiendelea.
==============================
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mkutano wa Wakuu wa Nchi kuadhimisha miaka 60 ya ushirikiano kati ya Asia na Afrika kufanyika Indonesia

Mkutano wa Maadhimisho ya Miaka 60 ya ushirikiano kati ya Asia na Afrika pamoja na Miaka 10 ya Mkakati Mpya wa Ubia Kati ya Asia na Afrika umeanza tarehe 19 Aprili 2015 hapa Jakarta, Indonesia.

Mkutano huo umetanguliwa na kikao cha Maafisa Waandamizi kinachojadili maazimio mbalimbali yaliyofikiwa mwaka 2005 pamoja na kutengeneza Agenda za Mkutano wa Ngazi ya Mawaziri na Wakuu wa Nchi na Serikali kuanzia tarehe 19 mpaka 24 Aprili 2015.

Kaulimbiu ya mkutano huu ni Kupanua wigo wa Ushirikiano kwa nchi wanachama “Advancing South - South Cooperation”.

Lengo kuu la mkutano huu ni kujadili kwa kina na kupitisha maazimio yatakayodumisha ushirikiano miongoni kwa nchi wanachama katika masuala ya ustawi wa amani, kuimarisha Mkakati Mpya wa Ubia kati ya Asia na Afrika na Azimio la Palestina. Maazimio yote hayo matatu yalijadiliwa na Maafisa Waandamizi kutoka Serikali za nchi wanachama na kisha kupitishwa na Mkutano wa Mawaziri.

Mkutano wa Wakuu wa nchi na Serikali utafanyika tarehe 22 na 23 Aprili 2015, ambapo Rais wa Jamhuri ya Indonesia, Mheshimiwa Joko Widodo anatarajiwa kuufungua kwa kutoa hotuba kwa wageni kabla ya kupitisha na kusaini Maazimio tajwa hapo juu.

Aidha, pamoja na mambo mengine, viongozi hao pia watajadili mustakabali mzima wa masuala mbalimbali yanayoendelea duniani katika Nyanja ya usalama, ubaguzi wa rangi, matabaka baina ya jamii, usafirishaji haramu wa binadamu, ugaidi na mengineyo. Siku ya mwisho, Mkutano unatarajia kukamilika kwa Wakuu wa nchi na Serikali kutembele jiji la kihistoria la Bandung ambako ndiko ulifanyika Mkutano wa kwanza wa ushirikiano kati ya Asia na Afrika miaka 60 iliyopita.

Ujumbe wa Serikali ya Tanzania kwenye mkutano huo, uliongozwa na Mheshimiwa Dkt Mary M. Nagu (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu, Balozi, Mbelwa Kairuki, Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Aziz Mlima, Balozi wa Tanzania nchini Indonesia mwenye makazi yake nchini Malaysia pamoja na Maafisa wengine katika taasisi hizo. 

Imetolewa na:
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Dar es Salaam
Tarehe 21 Aprili, 2015